Na Alex Wekesa
Rais William Ruto Jumamosi ,Juni 1,2024, ataongoza taifa la Kenya kuadhimisha siku kuu ya Madaraka dei.
Ni siku maalum inayoadhimishwa juni 1 kila mwaka kusherehekea uhuru wa ndani kwa ndani ,taifa la Kenya kujitawala kutoka mikononi mwa serikali ya mbeberu.
Kwa kawaida ,Madaraka dei husherehekewa katika sehemu mbalimbali nchini Kenya.
Wakenya hupata fursa kuonyesha ukomavu wa uhuru ,iweni kupitia nyimbo za kizalendo,za burudani na maonyesho na maigizo mbalimbali.
Maadhimisho ya mwaka huu wa ,2024, yatafanyika katika uga wa michezo wa Masinde Muliro, Kanduyi katika kaunti ya Bungoma.
Uwanja wa michezo wa Masinde Muliro, umekuwa ukikarabatiwa ili kuweza kutumika katika sherehe za Maadhimisho hayo.
Uwanja huo kwa zaidi ya miaka mingi iliyopita ,ulikuwa umetelekezwa na serikali kupitia idara husika.
Lakini baada ya Uwanja huo kuratibiwa kwa ajili ya maadhimisho hayo, serikali ya kaunti ilianzisha mpango wa kuukarabati.
Mwezi machi mwaka huu, serikali ya kaunti iliweza kuwasilisha uwanja huo kwa serikali ya kitaifa katika harakati ya ujenzi baada ya kutia mkataba ambao uliongozwa na waziri wa Michezo Ababu Namwamba na Gavana Kenneth Lusaka.
Waziri wa Michezo ,Ababu Namwamba, alisema kuwa hayo yalifanyika ili kuipiga jeki serikali ya kaunti katika kufanikisha ujenzi wa uwanja huo.
Waziri Namwamba alihakikisha kuwa pindi uwanja huo utakapomalizika kukarabatiwa utaregeshwa kwa serikali ya Kaunti.
Katika awamu ya pili ya ujenzi wa uga huo, Wanajeshi wa vikosi tofauti, walitumwa katika uwanja huo kwa ajili kukarabati, na kwa kweli wamesaidia pakubwa,kwani kufikia sasa uwanja huo umechukua sura mpya na unaweza kupigiwa mfano.
Uwanja huo ambao una uwezo wa kuwapokea wananchi zaidi ya elfu ishirini na tano, utavunja rekodi kuwahi kutumika katika shughuli za sherehe za Madaraka dei.
Uwanja huo ni wa kipekee kwani ulichukua jina la aliyekuwa mwanzilishi maarufu wa masuala ya kisiasa katika kaunti hii,Masinde Muliro ambaye aliaga dunia.
Akizuru hii leo na kufanya ukaguzi wa uwanja huo ,Waziri Ababu Namwamba, aliridhia kazi ambayo imefanyika katika uwanja huo,na kusema kuwa tayari umefika katika kiwango cha kuwapokea wageni katika sikukuu ya Madaraka dei.
Namwamba alisifia serikali ya Kenya Kwanza kwa kuhakikisha kuwa uwanja huo wa Masinde Muliro unakarabatiwa na kumalizika kwa wakati ufao.
Alidokeza kuwa ingawa haujaundwa vyema, ujenzi utaendelea hata baada ya Sherehe za Madaraka dei, ili kufanikisha Uwanja huo kuwa katika hadhi ya kimataifa.
Uwanja wa Masinde Muliro umejumuishwa kuwa miongoni mwa viwanja vitakavyokuwa wenyeji wa michuano ya CHAN na AFCON ambayo yameratibiwa kufanyika Novemba katika mwaka huu,2024.
Waziri Namwamba hata hivyo aliisuta serikali ya Jubilee kwa kutelekeza viwanja vya michezo nchini katika utawala wake, huku akiwahakikishia Wakenya kuwa serikali ya Kenya Kwanza kupitia wizara ya Michezo imejitolea ili kuona kuwa masuala ya michezo na talanta katika taifa hili yanapigwa jeki.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa kamati ya michezo katika bunge la kitaifa ambaye pia ni mbunge wa Webuye Magharibi, Dan Sitati Wanyama, ameeleza kujitolea kwa kamati hiyo kupasisha bajeti itakayosaidia kuendeleza katika shughuli za ujenzi wa uga wa Masinde Muliro.
Aidha Mbunge Wanyama, aliwarai wakazi wa Bungoma na Wakenya kwa jumla kujitokeza kwa wingi katika sikukuu ya Madaraka na kumlaki rais William Ruto ambaye atakuwa mgeni wa heshima wa Maadhimisho hayo.
Kadhalika,kamishna wa Bungoma, Thomas Sankei, aliwahikishia wananchi usalama wao kabla,wakati na baada ya sherehe za sikukuu ya Madaraka dei.



